Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema vijana 10,500
waliojitokeza hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufanya
usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ni ishara kuwa bomu la
ajira litalipuka muda wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya
Bunge, Lowassa alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa
kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali
nchini.
Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo
Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo.
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008,
amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo
la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.
Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye
malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na
suala la ajira kwa vijana.
Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna
Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye
alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora
watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania
sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu
na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,”
alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake,
huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya
pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria
kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,”
alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi
jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania
mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni
lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana
hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha
nne, cha sita na vyuo vikuu.
Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za
Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama
hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa
na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa
vijana.
Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema: “Vijana 10,500 kufanya usaili wa nafasi 70 ni
janga la taifa. Yupo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliwahi kulizungumza hili
lakini akapondwa kwamba anazungumza mambo kwa kuzua. Sasa huu ndiyo ukweli
wenyewe.”
Credit: Mwananchi
Post a Comment