0

VITAMBULISHO vya kupiga kura nchini, vitatolewa upya kwa wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura. Mchakato huo wa kutoa vitambulisho upya, utakaotekelezwa Septemba mwaka huu, utagharimu Sh bilioni 293 .

Tofauti na vitambulisho vya awali vya karatasi vilivyotolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, vipya vitakuwa vya plastiki. Vimebadilishwa kutokana na matumizi ya teknolojia mpya katika uandikishaji.

Teknolojia itakayotumika ni ya Biometric Voter Registration (BVR), ambayo inachukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika Kanzidata (database) kwa ajili ya utambuzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema hayo jana wakati akifungua mkutano kati ya tume na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kuhusu uboreshwaji wa daftari la wapiga kura.

Alisema katika uboreshaji huo, wapigakura wa zamani, kwa maana waliokuwa kwenye daftari la sasa, watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za vidole, picha na saini zao katika mfumo mpya wa BVR na hatimaye kupewa vitambulisho vipya.

Alisema vitambulisho hivyo vipya, vitatolewa papo hapo uandikishaji ukikamilika na vitakuwa vya plastiki ngumu na namba ya mpigakura itakayoonekana kwenye kitambulisho hicho, itakuwa ni ya kudumu na pekee kwa mpiga kura husika.

“Vitambulisho hivi vitatumika kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao pamoja na kura ya maoni ya Katiba mpya na kuhitimisha matumizi ya vitambulisho vya wapiga kura vya awali,” alisema Lubuva.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo kuhusu maandalizi hayo kwa kutumia mfumo wa BVR, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba alisema wapigakura watakaokuwa na kadi za zamani, watatakiwa kwenda na kadi hizo katika kituo cha kujiandikisha kurahisisha kuhamisha taarifa zao za awali katika mfumo mpya.

“Hata hivyo, kupotea ama kuharibika kwa kadi ya awali, hakumzuii mpiga kura kwenda kituoni kujiandikisha na kupewa kadi mpya,” alisema.

Wenye umri miaka 17 Alisema kundi lingine litakalohusika katika uboreshwaji huo ni watu ambao ifikapo siku ya uchaguzi mkuu mwakani, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18.

Pia, wale ambao hawakuwahi kujiandikisha katika madaftari yaliyopita kwa sababu mbalimbali, watahusika katika uboreshaji wa daftari.

Alisema baada ya kukamilika kwa uboreshwaji huo, daftari la awali litawekwa wazi katika maeneo husika na tarehe za ukaguzi, zitatangazwa ili kila aliyejiandikisha kwenda kukagua na kuona kama taarifa zake, zimeandikwa na kuchukuliwa kwa usahihi.

“Kipindi hicho pia kinatoa nafasi kwa wapigakura waliojiandikisha katika kata kuweka pingamizi kwa wale watakaoonekana wameandikishwa katika daftari lakini hawana sifa kama wasiokuwa raia au wasiotimiza umri unaotakiwa kisheria,” alisema.

Alisema matumizi ya mfumo wa BVR, yataweza kutoa majibu kwenye changamoto zilizojitokeza katika mifumo mingine iliyotangulia na kuwezesha kuondoa wapigakura, waliojiandikisha zaidi ya mara moja, kutambua wapigakura siku ya uchaguzi na kuhamisha wapigakura waliohama.

BVR ni uandikishaji tu Hata hivyo, Lubuva alisema mfumo huo wa BVR utatumika kwa ajili ya kuandikisha wapigakura pekee na si kwa ajili ya kupiga kura kielektroniki au vinginevyo.

Alisema matumizi ya mfumo huo, yametokana na changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya Optical Mark Recognition (OMR) na kufanya daftari la kudumu la wapigakura kuwa na kasoro na kusababisha wadau wa uchaguzi kuhoji uhalali wake.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lubuva alisema vifaa kwa ajili ya kazi hiyo vimekwishaagizwa. Tume itavipokea Agosti mwaka huu ili kuanza uboreshaji huo huku vifaa vichache kwa ajili ya mafunzo kwa watendaji vitapokewa mwezi Julai na kuanza mfunzo hayo.

Uandikisha kwenye vitongoji Alisema kwa sasa uandikishaji utafanyika katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa, tofauti na awali ambapo vilikuwa katika ngazi ya mtaa. Sasa vituo vya kujiandikishia, vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ili kuwa karibu na wananchi na kuongeza mwamko wa kujiandikisha na kupiga kura. Mchakato wa uandikishaji ukianza, huduma zitakuwepo kwa siku 14 kituoni.

Maandalizi Alisema maandalizi ya awali yamekamilika, kinachofuata ni mafunzo na kuanza uboreshwaji wa daftari utakaogharimu Sh bilioni 293 wanazopata kutoka serikalini na tayari sehemu ya fedha, wameshapokea na kutumika kukagua vituo .

Naibu Katibu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Tehama, Dk Sist Cariah, akizungumzia suala la vitambulisho vya taifa na hivi vya wapigakura, alisema vitambulisho hivyo ni tofauti kwani wao wanatoa kwa ajili ya kukamilika kwa muda maalumu lakini vile vya taifa ni endelevu.

Alisema kwa sasa, vitambulisho vya taifa hawajakamilisha kutoa hata Dar es Salaam pekee hivyo ni vigumu kutumika kwa uchaguzi ujao na kura ya maoni kwa Katiba mpya lakini wakikamilisha vitambulisho vya taifa , vitatumika katika uchaguzi.

Alisema katika mfumo huo mpya, watawasiliana na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuweza kuwaondoa wote waliofariki kwa kutumia takwimu za hospitalini na vyeti vya vifo vitakavyotolewa.


Source: Habari leo.

Post a Comment

 
Top