0


Mkutano wa 20 na wa Mwisho wa Bunge la 10 la Tanzania, unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, ambapo wabunge watajadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, pia maswali 295 ya msingi yataulizwa na kupewa majibu na hatimaye bunge hilo kuvunjwa rasmi Juni 27, mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Bunge, katika mkutano huo pia, maswali 56, yataulizwa kwa Waziri Mkuu ambapo pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ataweka mezani taarifa ya ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2013/14.

Aidha, bunge pia litajadili utekelezaji wa bajeti za wizara zote 24, kwa mwaka unaiosha wa 2014/15 na kujadili makadirio na matumizi ya Serikali kwa mwaka unaoanza wa 2015/16.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo hadi Jumamosi wiki hiii, baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge watapokea hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Uwekezaji na Uwezeshaji pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuijadili kwa siku hizo tano kabla ya kuipitisha.

Aidha, Mei 18, mwaka huu baada ya kipindi cha maswali na majibu hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, utawala bora, mahusiano na uratibu itawasilishwa na wabunge wataijadili kabla ya kuipitisha.

Ratiba ya uwasilishaji wa hotoba za wizara husika zitaendelea kwa mujibu wa tarehe husika na kwamba Juni 11, mwaka huu na hotuba ya Dira ya Nchi na Mipango itakayogusia taarifa ya hali ya uchumi wa nchi , ikifuatiwa na hotubaya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2015/16 itakayosomwa na Waziri wa Fedha.

//

Post a Comment

 
Top