Mamba 20 yaliyoachwa kwenye rasimu ya katiba - By PolePole
MAMBO 20 MUHIMU YA WANANCHI YALIYOTUPWA NA
KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
UNATAKA KUUJUA UKWELI BASI SOMA HAPA NA
MJULISHE MWENZIO.
Katiba Inayopendekezwa ina mapungufu
makubwa na imeyatupilia mbali maoni muhimu ya wananchi kama yalivyotolewa na
wananchi wenyewe kama ifuatavyo;-
1. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais Wananchi
walipendekeza madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe
Taasisi za kikatiba za kumshauri Rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi
walipendekeza pia baada ya Rais kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa huyo
Bunge limthibitishe. Katiba Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na imemuongezea
Rais Madaraka.
2. Kutenganisha Mamlaka ya Mihimili ya Dola
Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na Mamlaka zaidi kwa Bunge
kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali. Pendekezo hili linaenda
sambamba na kutenganisha serikali na Bunge, hali ambayo iko sasa. Rasimu ya
Warioba ililipa Bunge Mamlaka zaidi kuisimamia Serikali na hata pale ambapo
Bunge lingekataa bajeti au muswada mbaya wa serikali mara kadhaa, Rais
asingeliweza kulivunja Bunge. Wananchi walisema sana Mawaziri wasitokane na
wabunge, ili wabunge wafanye kazi ya uwakilishi pekee na mawaziri watumie
weledi wao kumsaidia Rais kazi za Serikali.
3. Kumwajibisha Mbunge Rasimu ya Warioba
iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa
na imani nao wakati wowote (Recall Powers) kama wakienda kinyume na maslahi ya
wananchi katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao,
iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze kumwajibisha
mpaka miaka mitano?
4. Vyanzo vya Mapato vya kuaminika Kuwepo
kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakavyogharimia
mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7 lilikuwa pendekezo
ambalo hata taasisi za serikali zilipendekeza. Pendekezo la Katiba
Inayopendekezwa imerudisha mapato ya Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977, na kwa
kufanya hivyo tumerudi kwenye mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa
forodha, ushuru wa bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na
kuifanya ishindwe kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na
vivyo hivyo kwa Tanganyika.
5. Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka
Kamili Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha ni muundo gani wa
Muungano Jamhuri yetu inao. Kitendawili hiki kimeelezwa na wengi akiwemo Baba
wa Taifa Mw. J.K Nyerere. Rasimu ya Warioba iliweka kwa mara ya kwanza Muundo
Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili na lenye
Serikali 3.
6. Kupunguza ukubwa wa Serikali Wananchi
walionesha kutofurahishwa na ukubwa wa serikali unaopelekea matumizi makubwa ya
fedha za walipa kodi. Walipendekeza uwepo wa serikali ya muungano iliyo imara,
yenye ufanisi na ndogo. Rasimu ya Warioba ilisema idadi ya mawaziri isizidi 15,
Katiba Inayopendekezwa inasema Mawaziri wasizidi 40
7. Tume ya Uhusiano na Uratibu Rasimu ya
Warioba ililenga kuhakikisha kunakuwepo uhusiano mzuri, mawasiliano na uratibu
wa serikali zote tatu chini ya Mamlaka ya Serikali ya Muungano na kupitia Tume
ya Uhusiano na Uratibu. Bunge Maalum lilishindwa kuelewa mantiki ya pendekezo
hili na Katiba Inayopendekezwa imelivuruga kabisa, kutoka pendekezo la Warioba
la “Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali” hadi “Tume ya Uratibu wa Mambo ya
Muungano” katika Katiba Inayopendekezwa.
8. Kupunguza ukubwa wa Bunge Wananchi
walizungumzia pia ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na gharama
zinazoambatana nalo, na wakapendeza bunge dogo na lenye ufanisi mkubwa. Warioba
alisema idadi ya wabunge isizidi 75, Bunge Maalum likasema Wabunge 390.
9. Ukomo wa vipindi vya ubunge Wananchi
walizungumzia nafasi za ubunge kuhodhiwa na watu fulani kwa miaka nenda rudi na
wakapendekeza ifike mahali kuwe na ukomo ili kuleta uwakilishi mpana na
mabadiliko. Rasimu ya Warioba iliweka ukomo wa vipindi vya ubunge kuwa vitatu
na kuwa na ukomo wa miaka 15 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Bunge Maalum na
Katiba Inayopendekezwa wamefuta pendekezo hili.
10. Kuwepo kwa Tunu za Taifa (Core Values)
Wananchi walipendekeza uwepo wa tunu za Taifa (core values) katika katiba, tunu
hizi ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha
ya Taifa. Raia wa Tanzania walikuwa na wajibu wa kuheshimu tunu hizi lakini
Katiba Inayopendekezwa imezifuta tunu hizi.
11. Maadili na Miiko ya Viongozi Wananchi
walizungumza kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya jamii, watumishi na
viongozi wa umma, wengi wakisema Katiba iainishe Maadili na miiko ya viongozi
wa umma ambayo kwayo tutawawajibisha. Katiba Inayopendekezwa imesema Maadili na
Miiko kwa viongozi (mathalani kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha
mgongano wa maslahi), isiwemo kwenye Katiba bali ikawekwe kwenye Sheria.
12. Masharti yasiyoweza kubadilishwa na
Bunge Rasimu ya Warioba iliweka masharti ya kuzuia Bunge kubadili baadhi ya
masharti mahususi ya Katiba (entrenched provision) ibara ya 119 isipokuwa kwa
ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni (mathalan Malengo Makuu ya Taifa, Haki
za Binadamu n.k. Na bahati mbaya tulisahau kuweka na Sura ya 3 juu ya Maadili).
Masharti yote ya Ibara hii yamefutwa isipokuwa Muundo wa Muungano na Uwepo wa
Jamhuri ya Muungano.
13. Kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi
Wananchi walizungumza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa
na jukumu la kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano. Ilisisitizwa juu ya
umuhimu wa Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kwamba Mwenyekiti wa Tume na
Makamu wake wathibitishwe na Bunge ili kuwapa uhalali wa kitaifa, pendekezo
hili limefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
14. Usawa wa 50:50 kati ya wanawake na
wanaume Kuwepo uwiano wa uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume ni
lazima kwa mazingira ya sasa. Uwiano kati ya wanawake na wanaume katika vyombo
mbalimbali vya dola hasa vile vya kutung sheria limeendelea kuwa tatizo nchini
na lililokaa kwa muda mrefu. Wananchi na hasa wanawake na baadhi ya wanaume
walipendekeza uwiano ulio sawa katika kufikia fursa hasa ukizingatia wanawake
ndio wazalishaji wakubwa. Katiba Inayopendekezwa imefutilia mbali pendekezo
hili muhimu.
15. Kuanzishwa kwa Mgombea Huru Haki ya
wananchi kushiriki shughuli za umma imekuwa ikizuiwa siku nyingi na kwamba
ushiriki katika shughuli za umma kama kiongozi wa kuchaguliwa inapaswa kuwa
haki ya msingi ya mwananchi yeyote yule. Rasimu ilitoa haki ya mgombea huru
bila vikwazo, Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti magumu ambayo hakuna mtu
anayeweza kuyatimiza kirahisi, kitendo hiki sio sawa.
16. Msaada wa Kisheria kwa Wananchi
Wananchi walieleza kutokuridhishwa kwao na huduma za msaada wa kisheria kwa
wananchi wenye uhitaji huo na wakapenda huduma ya msaada wa kisheria liwe suala
la kikatiba kwa mwananchi yeyote yule na serikali iwajibike kutoa huduma hiyo.
Katiba Inayopendekezwa imesema wananchi hawatakuwa na haki ya kudai huduma hii
kokote nchini, hata mahakama hazitaweza kusikiliza mashauri ama Serikali imetoa
haki hii au haikutoa haki hii rejea Ibara ya 21.
17. Uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Rasimu
ya Warioba ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa uhuru,
bila woga, upendeleo wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na
sheria za nchi. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa
18. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi
Tume ya Warioba ilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya
utumishi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba Inayopendekezwa
imefuta masharti haya licha ya wapiganaji kupendekeza utaratibu wa kusimamia
maslahi yao Kikatiba.
19. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la
kusimamia utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika uajiri wa askari wa Jeshi la
Polisi, Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni na misingi ya
utumishi iliyoainishwa katika Katiba hii
20. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi
Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake,
Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano litazingatia (a) viwango vya juu vya
kitaaluma na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake; (b) ulinzi na ukuzaji wa
haki za binadamu; (c) kanuni za uwazi na uwajibikaji; na (d) kukuza mahusiano
na jamii. Warioba akaendelea kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza
majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na kupambana na uhalifu
vya Nchi Washirika katika kufanya uchunguzi na kushughulikia makosa ya rushwa
na ufisadi. Misimefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
UKISOMA MPAKA HAPA HAKIKISHA NA MWENZAKO
ANAPATA UJUMBE HUU.
Post a Comment